SALA YA ASUBUHI
Ee Baba yetu Mungu mkuu, Umenilinda usiku huu, Nakushukuru kwa Moyo, Ee Baba, Mwana, na Roho. Nilinde tena siku hii, Niache dhambi, nikutii. Naomba sana, Baba wee, Baraka yako nipokee. Bikira safi, Ee Maria, nisipotee nisimamie, Mlinzi mkuu malaika wee. Kwa Mungu wetu niombee. Nitake nitende mema tu, na mwisho nije kwako juu. Amina.
NIA NJEMA
Kumheshimu Mungu wangu namtolea roho yangu, nifanye kazi nimpumzike, Amri zake tu nishike. Wazo, neno, tendo lote namtolea Mungu pote, Roho, mwili, chote changu, Pendo na uzima wangu, Mungu wangu nitampenda, wala dhambi sitatenda. Jina lako nasifia, utakalo hutimia, kwa utii navumilia, teso na matata pia. Nipe Bwana, neema zako niongeze sifa yako. Amina.
SALA YA MATOLEO
Ee Yesu, kwa mikono ya Bikira Maria, na kwa muungano na sadaka yako kuu, ninakutolea sala, matendo, masumbuko na furaha zangu zote za leo. Ee Yesu, ufalme wako utufikie.
BABA YETU
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALAMU MARIA
Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yuu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu, mzao wa tumbo lako, amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu,utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
KANUNI YA IMANI
Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, Muumba mbingu na dunia, Na kwa Yesu Kristo, Mwanae pekee, Bwana wetu, aliye tungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Akazaliwa na Bikira Maria, Akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa, Akashukia kuzimu, siku ya tatu akafufuka katika wafu, Akapaa Mbinguni, Amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi; Toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele. Amina.
AMRI ZA MUNGU
1. Ndimi Bwana Mungu wako, usiabudu Miungu wengine.
2. Usitaje bure jina la Mungu wako.
3. Shika Kitakatifu siku ya Mungu.
4. Waheshimu baba na mama, upate miaka mingi na heri duniani.
5. Usiue.
6. Usizini.
7. Usiibe.
8. Usiseme uwongo
9. Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10. Usitamani mali ya mtu mwingine.
AMRI ZA KANISA
1. Hudhuria Misa takatifu Dominica na sikukuu zilizoamriwa.
2. Funga siku ya jumatano ya majivu; usile nyama siku ya Ijumaa Kuu.
3. Ungama dhambi zako zote walau mara moja kila mwaka.
4. Pokea Ekaristi Takatifu hasa wakati wa Paska.
5. Saidia kanisa katoliki kwa zaka.
6. Shika sheria katoliki za ndoa.
SALA YA IMANI
Mungu wangu,nasadiki maneno yote linayosadiki, linayofundisha kanisa katoliki la Roma: kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo, wala hudanganyiki, wala udanganyi. Amina.
SALA YA MATUMAINI
Mungu wangu, natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristu, neema zako duniani na utukufu mbinguni, kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.
SALA YA MAPENDO
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote; kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu kama nafsi yangu kwa ajili yako. Amina.
SALA YA KUTUBU
Mungu wangu, nimetubu sana dhambi zangu, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza, wachukizwa na dhambi. Basi sitaki kukosa tena, nitafanya kitubio, naomba neema yako nipate kurudi. Amina
SALA KWA MALAIKA MLINZI
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili.
MALAIKA WA BWANA
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Salamu, Maria...........................................
Ndimi mtumishi wa Bwana.
Nitendewe ulivyonena.
Salamu, Maria...........................................
Neno la Mungu akatwaa mwili.
Akakaa kwetu.
Salamu, Maria...........................................
Utuombee, mzazi mtakatifu wa Mungu.
Tujalie ahadi za Kristu.
Tuombe
Tunakuomba Ee Bwana utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya malaika kwamba mwanao amejifanya mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu na ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.
MALKIA WA MBINGU (kipindi cha Pasaka)
Malkia wa mbingu furahi, Aleluya.
Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.
Amefufuka alivyosema, Aleluya.
Utuombee kwa Mungu, Aleluya.
Furahi, shangilia, ee Bikira Maria. Aleluya.
Kwani, hakika Bwana amefufuka. Aleluya.
Tuombe
Ee Mungu uliyependa kuifurahisha dunia, kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu Mwanao; Fanyiza twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.
TUNAUKIMBILIA
Tunaukimbilia, ulinzi wako, mzazi Mtakatifu wa Mungu, Usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuokoe kila tuingiapo hatarini, ee Bikira mtukufu mwenye baraka. Amina.
Comments
Post a Comment